Mke wa Rais na Mwenyekiti
wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo, WAMA, Mama Salma Kikwete akipokea tuzo ya
Millenium Development Goals, Women Progress Awards,2013, kutoka kwa Ms Jennie
Yeung , Rais wa Shirika la Sun Zhong Shan Foundation lililo chini ya United
Nations Education, Science, Cultural and Health Advancement Foundation la
nchini Marekani. Mama Salma alipokea tuzo hiyo baada ya kutimiza baadhi
ya malengo ya Millenia katika masuala ya ukimwi, elimu kwa watoto waliokosa
fursa na kuwawezesha wanawake kiuchumi nchini Tanzania. Kulia ni Katibu
wa WAMA, Ndugu Daud Nassib na kushoto ni Dr. Judy Kuriansky, Mhadhiri wa Chuo
Kikuu cha Columbia nchini Marekani.
…………………………………………………………………….
Na Anna Nkinda – New York
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete ametunukiwa
tuzo ya Malengo ya Maendeleo ya Milinia ya mwaka 2013 kwa wanawake na Shirika
la Voices of African Mothers (VAM) la nchini Marekani kutokana na kazi kubwa
anayoifanya ya kusaidia jamii wakiwemo wanawake na watoto.
Sherehe ya kukabidhi tuzo hizo zimefanyika
jana katika ukumbi wa mikutano uliopo makao makuu ya Umoja wa
Mataifa (UN) mjini New York.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa
Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) amekabidiwa tuzo hiyo kutokana na uongozi
wake madhubuti, mafanikio na mchango wake na kujitoa kwake kuwasaidia wanawake
na watoto wa Tanzania.
Akikabidhi tuzo hizo Nana – Fosu Randall
ambaye ni Rais na mwanzilishi wa shirika hilo alisema kuwa tathimini
ilitofanyika kwa mwaka 2012 juu ya Malengo ya Maendeleo ya Milenia
wametambua kwamba malengo matatu yamefikiwa nchini Tanzania kabla
ya muda uliowekwa wa kikomo wa mwaka 2015.
Alisema kuwa wake wa Marais wa Afrika
wanamajukumu mbalimbali katika nchi zao ili kufikia Malengo hayo, Taasisi ya
VAM imekuwa ikifanya tathimini juu ya hatua zilizofikiwa na Taasisi za wake wa
Marais kupitia taarifa za mwaka na zingine zinazowasilishwa.
“Wanawake hawa wanastahili kutuzwa
kwani wamefanya kazi kubwa pamoja na kufanya shughuli zao katika mazingira
yenye changamoto nyingi ukilinganisha na wenzao katika nchi zingine.
Hafla ya tuzo hizi siyo tu inasherehekea mafanikio
ya wake wa marais wa Afrika bali pia inawahamasisha na kuwatia moyo wakati huu
ambapo mwaka 2015 unakaribia”, alisema .
Alimalizia kwa kusema kuwa mara nyingi vyombo
vya habari vimekuwa vikiandika habari zisizokuwa sahihi kutokana na kazi
zinazofanywa na wake wa marais lakini vinasahau kuandika mambo mazuri na kazi
kubwa wanayoifanya ya kuwasaidia wananchi na kuviomba vyombo hivyo kubadilika
na kuthamini kazi kubwa wanayoifanya.
Akiongea mara baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo
Mama Kikwete alishukuru kwa tuzo aliyopewa na kusema kuwa Tanzania ni moja ya
nchi ambazo zimepiga hatua kubwa sana katika kufikia malengo ya milinia kwani
vifo vya watoto vimepungua kwa asilimia 45 na 49 kwa watoto wachanga.
Alisema kuwa haya ni mafanikio makubwa sana
japokuwa lengo ni kuondoa kabisa vifo ambavyo vinatokana na sababu ambazo
zinazuilika na katika malengo mengine maambukizi ya Virusi vya Ukimwi
(VVU) yanaendelea kupungua kutoka asilimia 5.7 kwa mwaka 2004 hadi asilimia 5.1
kwa mwaka 2011.
Mama Kikwete alisema, “Elimu ya msingi
inatolewa bure kwa watoto wote walio na umri unaostahili na hatua kubwa
imepigwa katika kupunguza ugonjwa wa maralia na vifo vya akina mama
vinavyotokana na tatizo la uzazi”
Kwa upande wa harakati za kumkomboa mtoto wa
kike alisema kuwa ni lazima ziendelee na zizingatie changamoto mpya za
mazingira mapya kwani unapompatia elimu unampunguzia changamoto za ujinsia na
kumpatia huduma ya afya ikiwemo uzazi wa mpango, unamuwezesha kushiriki zaidi
shughuli za maendeleo ya kiuchumi, unasaidia familia yake na jamii kuweza
kuendelea.
Kwa upande wake Dk. Judy Kuriansky ambaye ni
mwakilishi wa Asasi zisizo za Kiserikali zilizo chini ya UN alisema kuwa wake
wa marais wanafanya kazi kubwa ya kuisaidia jamii hivyo basi ni jukumu la kila
mmoja kuwaunga mkono na kushirikiana kwa pamoja ili kuweza kutimiza malengo ya
maendeleo ya milinia.
Dk. Kuriansky alisema kuwa ili kufikia
malengo ya milinia inatakiwa kuimarisha miundombinu iliyopo jambo ambalo
litasababisha kuifikia jamii kwa ukaribu zaidi na kuweza kutatua changamoto
zinazowakabili.
Tuzo hizo zimetolewa kwa mara ya kwanza na
shirika hilo kwa kushirikiana na Taasisi ya The reed for Hope (RFHF) na
Bethesda Counsel kwa wake wa marais wa Afrika akiwemo Mke wa Rais wa Burundi
Mama Dk. Denice Nkurunziza, Mke wa Rais wa Equatorial Guinea Mama Mintou
Doucoure Epse Traore na Mke wa Rais wa Mali Mama Dk. Malika
Issoufou.
0 comments:
Post a Comment