Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni Freeman Mbowe.
Naibu Spika wa Bunge Job Ndugai
Kitendo
cha Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, kukataa kumpa nafasi Kiongozi wa Kambi ya
Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe na kuwaamuru askari kumtoa kwa nguvu, lakini
pia kiongozi huyo kugoma kutii amri ya kiti, na hivyo kuzua vurugu bungeni
kimeibua hisia na maoni tofauti kutoka kwa wachambuzi mbalimbali.
Baadhi ya wachambuzi wa sayansi ya
kisiasa pamoja na wafuatiliaji wa mambo, wamezungumzia tukio hilo kuwa
linajengwa na sura mbili ya ukaidi na udhaifu wa kiti cha Spika.
Ni kwa namna hiyo wamemtaja Ndugai
moja kwa moja kuwa pengine anaponzwa na ujasiri alionao lakini pia kushindwa
kwake kutumia busara wakati wa kufanya maamuzi ya kiti.
Wakati Ndugai akishutumiwa kwa namna
hiyo, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe naye amenyooshewa
kidole lakini kwa sura tofauti na ile ya Ndugai.
Hatua hiyo inakuja ikiwa ni siku chache, baada ya vurugu kubwa
pengine kuliko zote zilizowahi kutokea bungeni, ambazo chanzo chake ni pale
Mbowe aliposimama na Ndugai kushindwa kumpa nafasi ya kuzungumza alichotaka
kusema badala yake akamuamuru kukaa chini kabla hajawaita askari kumtoa.
Ikiwa ni mwendelezo wa vurugu
zilizowahi kutokea bungeni siku za nyuma, wachambuzi hao wameanza kupata shaka
na hata kuanza kuhoji ni kwanini matatizo mengi yanapotokea bungeni chanzo
chake huwa ni kiti ambacho wakati huo huwa kimekaliwa na Ndugai.
Wanaoliona hilo wanamzungumzia
Ndugai kwamba huenda anaponzwa na ujasiri wake wa kiti kuliko kutumia busara.
Wanahoji alikoupata ujasiri Ndugai
wakati ambapo Tanzania inafuata mfumo wa Kibunge wa Jumuiya ya Madola unaotoa
fursa sawa kwa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani na Waziri Mkuu.
Wakati haya yakitokea sasa,
wachambuzi hao wameanza kuupima utendaji wa Ndugai kwa namna ya kuangalia idadi
ya matukio ambayo yamekuwa yakivuruga mwenendo wa Bunge wakati yeye akiwa
amekalia kiti.
Katika
hilo, itakumbukwa kuwa Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema), aliwahi
kufukuzwa bungeni na Ndugai baada ya kutamka kuwa Rais Jakaya Kikwete ni
dhaifu.
Mbali na hilo, Mei 30 mwaka huu,
Ndugai alilazimika kuahirisha Bunge mara mbili na kusitisha hotuba ya Bajeti ya
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa baada ya wabunge wa CUF,
kumchachamalia Mbunge wa Nyamagana, Ezekiah Wenje (Chadema), ambaye alisema
msimamo wa kiliberali wanaoufuata CUF unashabikia ushoga na usagaji.
Ni kwa mwenendo huo wa utendaji wa
Ndugai, Mwanasheria maarufu nchini, Majura Magafu, ameeleza kushangazwa na
mwenendo wa Naibu Spika huyo huku akihoji kuwapo kwa mlolongo wa mizozo
inayoibuka ndani ya Bunge wakati anapoongoza vikao.
“Huwa najiuliza maswali mengi, ni
kwanini kila wakati Ndugai akiwa kwenye kiti kunatokea mzozo? Hapa ni dhahiri
kuwa kuna udhaifu mkubwa na hata kwa kiti kizima cha spika, wameshindwa
kuendesha Bunge na hata wabunge wenyewe hawajiheshimu,”alisema.
Alieleza kuwa siku zote hakuna aliye
juu ya sheria, hivyo kitendo cha Mbowe kukaidi amri ya Naibu spika nayo ni
kukiuka sheria.
“Wabunge
watambue kuwa Bunge ni sehemu inayoheshimika na inastahili ipewe heshima.
Pia watambue kuwa Bunge haliongozwi kama klabu ya pombe bali kuna kanuni
na sheria.
“Mbunge na Spika wanapokiuka kanuni
wanakuwa hawawatendei haki Watanzania na hawajatumwa bungeni kwenda kutukanana
na kupigana bali kutatua matatizo ya wananchi,” alisema Magafu.
Kwa upande wake, Mwanasheria, Peter
Kibatala, alisema Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, hadhi yake ni sawa na
Waziri Mkuu, hivyo hata kama amekosea hatakiwi kuamriwa kama wabunge wengine,
bali kiti cha spika kinatakiwa kitumie staha.
“Kuna namna ya ‘kum-handle’ Kiongozi wa Kambi ya Upinzani
Bungeni tofauti na wabunge wengine. Ndugai alitakiwa kutumia busara ya kipekee
si kama alivyofanya na ndiyo maana yakatokea yote yale,”alisema Kibatala.
Mwanasheria nguli nchini, Masumbuko
Lamwai, alisema ni dhahiri kwamba Ndugai si kiongozi kwa kuwa kila fujo
inapotokea bungeni yeye anakuwa kwenye kiti.
“Kiongozi wa Kambi ya Upinzani ni tofauti na wabunge wengine
mfano angesimama Waziri Mkuu wangemwambia akae chini?,”alihoji Lamwai.
Alipoulizwa na gazeti hili endapo ni
sahihi kwa kitendo cha Mbowe kukaidi amri ya Naibu Spika, alisema suala
lililokuwa linazungumzwa lilikuwa kubwa hivyo alitakiwa kusikilizwa.
“Ndugai aachie ile nafasi haimfai na
waliomchagua hawakuchagua kiongozi. Ile issue ilikuwa hot hivyo alitakiwa
kutumia busara na uongozi wakati mwingine ni busara si sheria,”alisema Lamwai.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, Bashiru Ali, alisema kilichotokea bungeni ni kawaida na inaweza kutokea
hata nje ya Bunge kwa kuwa watu hawataki kufikia muafaka wa namna ya kupata
Katiba.
“Tunatakiwa tuangalie chanzo na si
kilichotokea bungeni na tunaweza kushuhudia vurugu kama zile hata nje ya Bunge.
Waliofanya vile ni wale wenye wasiwasi kuhusu mchakato wa Katiba kutokana na
mwenendo wake,”alisema Bashiru Ali.
Naye Mwanasheria Mabere Marando alisema Kiongozi wa Kambi ya
Upinzani anaposimama bungeni hata kama kuna mbunge anazungumza anatakiwa
asikilizwe kama alivyo kwa Waziri Mkuu.
Source: Hombo E. (Sept. 2013)Retrieved from Mtanzania
0 comments:
Post a Comment