Kamishina wa Nishati na Masuala ya Petroli toka Wizara ya Nishati na Madini Mhandisi Hosea Mbise akizungumza na waandishi wa habari kuhusu faida zitokanazo na gesi asilia, kushoto ni Mhandisi Seleman Khatib anayehusika na Nishati na kulia ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya habari Zamaradi Kawawa akifuatiwa na Kaimu mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano toka Wizara ya Nishati na Madini Veronica Simba PICHA NA ELIPHACE MARWA (MAELEZO).
FAIDA ZITOKANAZO NA GESI ASILIA NCHINI
Utafiti wa mafuta na gesi nchini ulianza tangu mwaka 1952 chini ya kampuni za BP na Shell. Hadi sasa kampuni zipatazo 19 zinaendelea na utafiti katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo maeneo ya kina kirefu cha maji baharini, mwambao wa bahari, na katika bonde la ufa.
Kiasi cha Gesi Asilia iliyogunduliwa nchini Tanzania, inakadiriwa kufikia futi za ujazo trilioni 41.7, kati ya hizo, zaidi ya futi za ujazo trilioni 33 zimegunduliwa katika kina kirefu cha maji baharini. Uhakiki wa gesi hii pamoja na utafiti unaendelea na mategemeo makubwa ni kuendelea kugundua gesi zaidi na pia hata mafuta.
Kawaida, Gesi Asilia inaweza kutumika kama nishati (energy) na vile vile inatumika kama malighafi (feedstock) katika baadhi ya viwanda (Gesi asilia inatumika kutengeneza Mbolea, Plastics, Methanol pamoja na kemikali nyingine nyingi) na pia ya kuuzwa nje ya nchi kama bidhaa (export commodity).
1.1. Faida zilizopatikana kutokana na Gesi Asilia Nchini
Faida halisi zilizopatikana kutokana na matumizi ya Gesi Asilia nchini ni ni pamoja na zifuatazo:
Sekta ya umeme
Sekta ya umeme ilianza kutumia Gesi Asilia tangu mwezi Julai, 2004, hadi sasa kiasi cha megawati (MW) 418.5 huzalishwa nchini kwa kutumia nishati hiyo. Takriban Dola za Marekani Bilioni 4.4, sawa na Shilingi za Tanzania Trilioni 7, zimeokolewa kwa kutumia gesi asilia kufua umeme kuanzia Julai 2004 mpaka Machi 2013.
Sekta ya Viwanda.
Gesi Asilia inatumika katika viwanda 37 vilivyopo Dar es Salaam. Takwimu zinaonyesha kuwa, viwanda 37 vinavyotumia Gesi Asilia, vimepunguza gharama za nishati kwa kiasi cha zaidi ya Dola za Marekani Milioni 400, sawa na shilingi bilioni 640, ikilinganishwa na kama vingetumia mafuta katika kuendesha mitambo yao kwa kipindi cha kuanzia Julai, 2004 hadi Disemba, 2012.
Sekta ya Usafiri
Hadi sasa, magari 40 yamewekewa mfumo wa kutumia gesi asilia. Mfumo huu unatumika sambamba na mfumo wa mafuta ya petroli uliopo kwenye magari. Kwa kipindi cha kuanzia Mei, 2011 hadi Machi, 2013 magari hayo yametumia gesi yenye thamani ya Shilingi milioni 22.88. Kwa kipindi sawa na hicho, magari hayo yangetumia mafuta ya petroli yenye thamani ya shilingi milioni 46.2. Hivyo, fedha iliyookolewa kwa magari 40 kutumia gesi asilia badala ya mafuta ya petroli kwa kipindi hicho ni shilingi milioni 23.32.
Mapato Serikalini.
Kuanzia Julai, 2004 hadi Machi, 2013, Serikali iliweza kukusanya jumla ya Dola za Marekani milioni 201.2, sawa na shilingi bilioni 321.9 kutokana na kodi ya ongezeko la thamani (VAT) pamoja na mauzo ya gesi asilia.
Mapato kwa Halmashauri za Kilwa (Lindi) na Mtwara Vijijini (Mtwara)
Sheria inazitaka kampuni zinazozalisha na kuuza Gesi Asilia kulipa Kodi ya Huduma (Service Levy), ambayo ni asilimia 0.3 ya mauzo ya Gesi Asilia. Fedha hizi hulipwa kila baada ya uzalishaji wa kipindi cha miezi mitatu (robo mwaka). Halmashauri zinazofaidika na mapato hayo ni Kilwa (Lindi) kutokana na mradi wa Songo Songo na Mtwara Vijijini (Mtwara) kutoka mradi wa Mnazi Bay.
Kuanzia kipindi cha mwezi Julai, 2004 mpaka Disemba, 2012, jumla ya kiasi cha shilingi milioni 885 zimelipwa kwa Halmashauri ya Kilwa kama kodi ya huduma (service levy), kwa wastani wa takribani shilingi milioni 109 kila baada ya miezi mitatu.
Kwa upande wa mradi wa Mnazi Bay, Halmashauri ya Mtwara Vijijini hupata wastani wa shilingi milioni 16 kila mwaka. Kiasi hiki ni kidogo sana kutokana na uzalishaji na uuzaji mdogo wa gesi ingawa visima vilivyopo Mnazi Bay vina uwezo wa kuzalisha gesi nyingi zaidi.
Kufuatia hazina kubwa ya gesi asilia iliyogunduliwa katika kina kirefu cha maji baharini, Serikali pamoja na kampuni zilizowekeza kwenye utafutaji zimeamua kuwekeza katika uzalishaji mkubwa wa Gesi Asilia ili kuleta tija zaidi kwa Taifa na watu wake.
Aidha, miradi yote ya gesi kama nishati, viwanda, mitambo ya kufua umeme pamoja na viwanda vya petrochemicals, kwa kiasi kikubwa vinategemea kukamilika kwa ujenzi wa mradi wa miundombinu ya kusafisha na kusafirisha gesi asilia kutoka Mnazi Bay (Mtwara) na Songo Songo (Lindi) hadi Dar es Salaam.
IMETOLEWA NA:
WIZARA YA NISHATI NA MADINI
19 JULAI, 2013
0 comments:
Post a Comment