Simba na Yanga zitakutana kwa mara ya kwanza katika mechi ya watani wa jadi msimu huu Oktoba 20 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, kwa mujibu wa ratiba mpya ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara 2013-14 iliyotolewa jana na shirikisho la soka nchini (TFF).
Miamba hao wa soka nchini walipokutana kwa mara mwisho katika mechi ya kufunga msimu uliopita Mei 26 mwaka huu, Yanga iliwafunga Wekundu wa Msimbazi kwa magoli 2-0 huku Wanajangwani wakiwa tayari walishatwaa ubingwa wa ligi kutoka mahasimu wao hao.
Akizungumza jana jijini, Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, alisema kuwa timu hizo kongwe zitakutana katika mechi yao ya marudiano Aprili 27 mwakani ikiwa ndiyo siku ya funga dimba ya msimu huo.
Osiah alisema siku ya ufunguzi wa ligi hiyo itakayoanza Agosti 24 mwaka huu, timu zote 14 zitakuwa viwanjani na kuongeza kuwa mzunguko wa kwanza utamalizika Novemba 3 mwaka huu.
Alisema kuwa mechi hizo za ufunguzi zitatanguliwa na mchezo wa kufungua msimu maarufu Ngao ya Jamii utakaowakutanisha mabingwa watetezi Yanga dhidi ya washindi wa pili, Azam zote za jijini Dar es Saalam Agosti 17 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa.Pia kiongozi huyo aliwataka viongozi wa klabu zinazoshiriki ligi hiyo kuzingatia kanuni na taratibu za usajili huku akisisitiza kwamba klabu zinatakiwa ziwe na viwanja maalumu vya kufanyia mazoezi.
Alieleza pia bado TFF iko katika mazungumzo na kampuni moja kwa ajili ya kuwa mdhamini mshiriki wa ligi hiyo.
Alizitaja mechi za ufunguzi wa ligi hiyo zitakuwa ni kati ya Yanga dhidi ya Ashanti United (Uwanja wa Taifa), Mtibwa Sugar dhidi ya Azam (Uwanja wa Manungu, Morogoro), na JKT Oljoro itakayowakaribisha Coastal Union kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha.
Mechi nyingine za siku hiyo ya fungua dimba zitakuwa ni kati ya Mgambo Shooting dhidi ya JKT Ruvu jijini Tanga, Rhino Rangers dhidi ya Simba (Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora), Mbeya City na Kagera Sugar (Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine, Mbeya) wakati Ruvu Shooting na Tanzania Prisons zitapambana kwenye Uwanja wa Mabatini Mlandizi mkoani Pwani.
Hata hivyo, Osiah aliwataka wamiliki wa viwanja vitakavyotumika katika ligi kuvifanyia marekebisho na hatimaye kufikia ubora unaotakiwa kwa ajili ya kulinda usalama wa wachezaji.
“Ni Uwanja wa Taifa na wa Azam Complex pekee ndivyo viko kwenye hali nzuri,” alisema Osiah.
Aliongeza kuwa Ligi Daraja la Kwanza Ngazi ya Taifa itaanza Septemba 14 na itaanza kwa hatua ya makundi.
Naye Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF, Saad Kawemba, alisema kuwa ratiba hiyo iliyotolewa imezingatia ushiriki wa Yanga na Azam katika mashindano ya kimataifa na endapo watatolewa mapema itafanyiwa marekebisho.
Alisema pia klabu ambazo zitakuwa zimesajili wachezaji pungufu ya 24 wataruhusiwa kuongeza katika kipindi cha kati ya Agosti 12 na 30 mwaka huu lakini wachezaji watakaosajiliwa watoke nje ya timu zinazoshiriki ligi hiyo.
0 comments:
Post a Comment