Breaking News

Tuesday

WAANDISHI WASITUMIWE KAMA DODOKI

"...kutumia waandishi wa habari kama vipaza sauti vya serikali; kukuza, kutia chumvi, kuficha ukweli na hata kusema uongo, ni kudhalilisha taaluma; ni kutubana na kututanua kama anayechezesha mwanasesere."

Neville,
Hii uliyoandika (Mabadiliko 3 Julai 2013), naipachika hapa chini, sikubaliani nayo:

Nukuu:
"1. Udhaifu wa kwanza hata Ikulu ilishindwa kumwandaa Rais kuzungumza na dunia maswala makubwa ya nchi yetu ambayo tunadhani yangetupa nafasi ya kutambulika kwamba sisi ni akina nani. Hili lingeweza kufany
ika hata kwa KUPANDIKIZA maswali ya msingi kwa Waandishi wa Habari wa Tanzania na kuhakikisha wanapata nafasi ya kuyauliza."
Mwisho wa nukuu.

Hii siitaki. Kutumia waandishi wa habari wa hapa nchini kuuliza maswali ambayo yatawaonyesha wageni kuwa "sisi ni akina nani?" Neville, "kupandikiza maswali ya msingi" ili dunia ituelewe sisi ni akina nani ? Hili, sikubaliani nalo.

Kwanza, kitu gani Marekani haifahamu juu ya Tanzania ? Ubalozi wake uko hapa na wafanyakazi kibao, wakikusanya taarifa kana kwamba wana vyombo vya habari. Wanatumia pia wenyeji kutafsiri yaliyoandikwa magazetini na kukalimani yanayotangazwa redioni na kwenye TV. 

Wanakutana na viongozi wakuu na wadogo serikalini, wafanyabiashara wakubwa, watumishi mbalimbali, viongozi wa asasi za kijamii, viongozi wa upinzani na wananchi wa kawaida. 

Kitu gani hawajui ? Ni hivi, kwa maana ya taarifa za kawaida na taarifa za kijasusi, Marekani inajua hata kipele kilichoko kwenye mwili wa rais wetu na sehemu kilipo. Kutumia waandishi kusema unachotaka, kutafanya waandishi waonekane wa ovyo na wasiojua kazi zao.

Pili, kutumia waandishi wa habari kama vipaza sauti vya serikali; kukuza, kutia chumvi, kuficha ukweli na hata kusema uongo, ni kudhalilisha taaluma; ni kutubana na kututanua kama anayechezesha mwanasesere. Hili halikubaliki. Kwa hiyo, ikulu (kwa maana ya serikali), itafute njia zake za kujieleza kwa wageni; ambao "bahati mbaya," wanajua mengi, hata mlo wetu wa jana.

Tatu, kukosekana kwa waandishi wa habari wengi wa Tanzania kuuliza maswali, kunaweza kutokana na mambo mawili: Utaratibu uliowekwa wa kuinua waulizaji; na udhaifu wa waandishi wenyewe. Katika mazingira ya rais wa Marekani, kunahitajika "ushapu" hata wa kuvunja protokali - poteleambali! Hawawezi kukukamata. 

Najua wakikukamata, watakuachia baadaye. Hawakujui - itakuwa kashfa ya karne. Unasimama haraka na ghafla na kuweka swali lako: "Mheshimiwa Kikwete umemwambia Rais Obama kuwa kasi ya kuua raia imeongezeka na kwamba hivi sasa kazi ya polisi inafanywa na jeshi la wananchi; ikiwa ina maana kwamba utawala umekushinda?"

Unafahamu ? Rais (mwanasiasa) aweza kujibu kwa njia mbalimbali. Wana jeuri hawa. Kwa mfano aweza kujibu, "Ehe! swali jingine!" Akakuacha solemba. Au, "Tumeongea mengi. Hilo utaniuliza baada ya mgeni kuondoka." Huwezi kuongeza swali kwani "muda hautoshi" na mwingine atakuwa ameanza kuuliza lake. Unahitajika ujasiri hata wa kuhimili jeuri ya wakubwa!

Nne, kuuliza katika lugha "mbovu" si hoja sana. Kama swali lina mantiki, ni mantiki hiyo itakayoliongezea uzito na hadhi mpaka kila mmoja akaona linastahili kujibiwa. Bali, ili kuondokana na kutoeleweka, hasa katika mazingira ya kasi kama hayo, siyo vibaya kuandika swali lako, tena kwa ufupi.

Ni vizuri kujua lugha za watu wengine, lakini kutojua kufikia "viwango vya Malikia" - kwani lugha ni utamaduni -  kusikufanye ujikunyate na ushindwe kutoa dukuduku lako. 

Hata hivyo, wahusika wanapaswa kuweka wakalimani ili yeyote aweze kuuliza kwa wepesi, katika lugha yake, huku waliobobea katika lugha hizo wakiwasilisha kwa lugha ya mlengwa.

Hata kwa upande wa rais, siyo sahihi kulazimisha matumizi ya lugha ya kigeni (Kiingereza) wakati anaelewa vema lugha yake. Hilo nalo liwe funzo.
CHANZO http://ndimara.blogspot.com
Share:

0 comments:

Post a Comment

Chapisho Lililoangaziwa

WEDDING PARTY PHILLIPO AND LUSIO

PHILLIPO & LUSIO WEDDING PARTY: STILL PICTURE, VIDEO SHOOTING MC & MUSIC BY MC SIMBA COMPANY 0715 501 059

Jumla ya Mara Iliyotazamwa

Powered by Blogger.

Pages