RAIS KIKWETE WA TANZANIA
RAIS KAGAME WA RWANDA
DAR ES SALAAM.KWA mara ya kwanza Rais Jakaya Kikwete amemtolea uvivu Rais wa Rwanda, Paul Kagame kutokana na kitendo chake cha kumtolea lugha za matusi baada ya kumshauri kukaa meza moja na vikundi vya waasi wa nchi yake (FDLR), huku akimtaka kuacha kukuza mgogoro usiokuwepo.
Rais Kikwete alitoa ushauri huo kwa Rwanda takribani miezi miwili iliyopita wakati akizungumza katika kikao cha Mkutano wa Umoja wa Afrika (AU) uliofanyika mapema mwaka huu, mjini Addis Ababa, Ethiopia, ambao ulikuwa ukij
adili suala la amani ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) pamoja na Ukanda wa Maziwa Makuu.
Ushauri huo pia uliwagusa Rais Yoweri Museveni wa Uganda na Joseph Kabila (DRC), ambao aliwataka kufanya mazungumzo na waasi wanaopingana na Serikali zao.
Akizungumza katika hotuba yake ya kila mwezi Rais Kikwete alisema: “Ushauri ule niliutoa kwa nia njema kabisa, kwani bado naamini kuwa kama jambo linaweza kumalizwa kwa njia ya mazungumzo njia hiyo ni vyema itumike,”
“Isitoshe, ushauri ule niliutoa pia kwa Serikali ya Congo , Serikali ya Uganda. Katika mkutano ule Rais Museveni wa Uganda aliunga mkono kauli yangu. Rais Kagame hakusema chochote pale mkutanoni. Baada ya kurudi nyumbani ndipo tukaanza kuyasikia maneno tuliyoyasikia na tunayoendelea kuyasikia.”
Alisisitiza, “Kwa upande wangu sijasema lolote kuhusu Rwanda pamoja na maneno mengi ya matusi na kejeli yanayotoka kwenye vinywa vya viongozi wa Rwanda dhidi yangu. Siyo kwamba siambiwi yanayosemwa au sijui kusema au sina la kusema, la hasha, sijafanya hivyo kwa sababu sioni faida yake.”
Rais Kagame alitoa lugha zisizostahili dhidi ya Rais Kikwete katika sherehe ya kuhitimu mafunzo ya kijeshi ya maofisa 45 wa jeshi lake Julai mwaka huu, ambapo alisema ushauri wa kufanya mazungumzo na waasi wa FDLR ni ujinga na haupo katika historia ya Wanyarwanda.
“Nilinyamaza kimya kwa sababu sikupenda kusikiliza ushauri kuhusu FDLR, kwa sababu nafikiri ni upuuzi ulioambatana na ujinga. Hatuwezi kuacha maisha yetu kama Wanyarwanda tunavyoishi sasa. Ushauri wa Kikwete ni sawa na kucheza na makaburi ya watu wengi ambao ni ndugu zetu,” alisema Kagame.
Katika hotuba ya jana Rais Kikwete alisema uhusiano wa Tanzania na Rwanda unapitia katika wakati mgumu na mtikisiko, baada ya yeye kutoa ushauri kwa Serikali ya Rwanda kuzungumza na mahasimu wao na kwamba hilo linadhihirika katika kauli zinazotolewa na viongozi wa Rwanda.
“Napenda kuwahakikishia Watanzania wenzangu na ndugu zetu wa Rwanda kuwa mimi, Serikali ninayoiongoza na wananchi wa Tanzania ,tunapenda kuwa na uhusiano mzuri na ushirikiano wa karibu na Rwanda kama ilivyo kwa nchi zote jirani” alisema Rais Kikwete.
Alisema nchi hizo ni jirani na kila moja inamuhitaji mwenzake, hivyo lazima ziwe na uhusiano mwema na ushirikiano mzuri.
“Nasisitiza kuwa mimi na Serikali ninayoiongoza tutakuwa wa mwisho kufanya kitendo au vitendo vibaya dhidi ya Rwanda au nchi yoyote jirani au yoyote duniani. Hatuna sababu ya kufanya hivyo, kwani ni mambo ambayo hayana tija wala masilahi kwetu” alisema.
Alisema nchi hizo mbili zimekuwa zikijihusisha na mambo ya kukuza na kujenga ujirani mwema, kusisitiza kwamba hiyo ni moja ya nguzo kuu ya Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania. MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment