Msimamizi wa Mradi wa Bara bara tatu za Vijijini za Unguja kutoka Wizara ya Miundo Mbinu na Mawasiliano Mhandisi Suleiman Abdulla Ali akimpatia maelezo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyetembelea mradi huo katika Bara bara ya Cheju – Jendele – Kaebeona.Kati kati yao aliyevaa kofia ya Kiua ni Waziri wa Wizara hiyo Rasdhid Seif na pembeni ya Mhandisi Suleiman ni Mshauri Muelekezi waMradi huo Kutoka Kampuni ya Newtech Consulting Group ya Nchini Sudan El- Tayeb Rabah Mohammed.
Mshauri
Muelekezi wa Mradi huo Kutoka Kampuni ya Newtech Consulting Group ya Nchini
Sudan El- Tayeb Rabah Mohammed akimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif ujenzi wa bara bara zenye kiwango katika mradi wa
bara bara tatu za Vijiji za Unguja huko Cheju Wilaya ya Kati, Mkoa Kusini
Unguja.Picha na Hassan Issa-Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar
--
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewaagiza wataalamu wanaopata
fursa za Ujenzi wa Bara Bara Nchini kuhakikisha kwamba bara bara wanazozijenga
zinakuwa katika kiwango kinachokubakila Kimataifa ili ziwe na uwezo wa kudumu
kwa kipindi kirefu.
Agizo
hilo amelitoa wakati wa ziara fupi ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Bara bara
ya Jendele-Cheju hadi Kaibona yenye urefu wa Kilo mita 11.741 ambayo ni
miongoni mwa bara bara iliyomo ndani ya mradi wa ujenzi wa bara bara tatu
za vijijini katika Kisiwa cha Unguja.
Balozi
Seif alisema wapo baadhi ya wahandisi wa ujenzi wa Bara bara wasio waaminifu
ambao baadhi ya wakati hudiriki kuondoa njiani miradi ya ujenzi wa bara bara
wanayopewa bila ya kuzingatia masharti na mikataba waliyoiridhia.
Alisema
hali hiyo huleta kero kwa wafadhi wa miradi hiyo na mara nyingi kuyatia hasara
Mataifa yenye miradi hiyo ambayo mengine yanashindwa kuihudumia Miradi husika
kutokana na ufinyu wa uchumi wao.
“Baadhi
ya Makandarasi wamekuwa na tabia ya kuondosha njiani kazi wanazopewa za
ujenzi tabia ambayo huwakera wafadhili wa miradi hiyo na kwa upande mwengine
kuyaongezea mzigo Mataifa yenye kusaidiwa ufadhili wa miradi hiyo “.
Alisisitiza Balozi Seif.
Akizungumzia
suala la fidia ya vipando, mali pamoja na majengo ya wananchi wanaoathirika na
miradi hiyo Balozi Seif aliiagiza Wizara ya Miundo Mbinu na Mawasiliano
Zanzibar kuwa makini ya baadhi ya watu wajanja wenye tabia ya kujipandikiza
katika madai ya fidia hizo.
Alisema
tabia hiyo ambayo hujichomoza mara kwa mara wakati wa uanzishwaji wa miradi
tofauti katika maeneo mbali mbali Nchini imekuwa ikiitia hasara kubwa Serikali
kwa vile haimo ndani ya jabeti iliyokubalika kwa pande zote mbili.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliipongeza Kampuni ya ujenzi wa Bara bara hiyo ya
D.P Shapriya +Co. Ltd ya Dara es salaam kwa hatua iliyofikia ya ujenzi wa mradi
huo licha ya kuchelewa kidogo kutokana na msimu wa mvua za masika.
Mapema
Msimamizi wa Mradi huo wa Bara bara tatu za Vijijini Unguja kutoka Wizara ya
Miundo Mbinu na Mawasiliano Zanzibar Mhandisi Suleiman Abdulla Ali alisema
Serikali kupitia Wizara husika tayari imeshawalipa fidia wananchi wote
waliohusika na ile bara bara ya Jendele- Cheju- hadi Kaebona.
Mhandisi
Suleiman alimueleza Balozi Seif kwamba tathmini ya fidia imeshafanywa pia kwa
bara bara ya Koani – Jumbi yenye urefu wa Kilo Mita 6.3 kwa kushirikiana na
masheha wa shehia zinazopita bara bara hiyo na Wizara husika italipa fidia mara
tuu fedha zitakapopatikana.
Alifahamisha
kwamba ufinyu wa bajeti ya kazi za ujenzi wa Bara bara hizo za Vijijini Unguja
umepelekea kutolewa kwenye mradi huo kwa Bara bara ya Kizimbani – Kiboje yenye
kilo mita 7.
Msimamizi
huyo wa mradi wa ujenzi wa bara bara hizo alieleza kuwa ujenzi wa kazi hiyo
ulioanza mapema mwezi Januari mwaka huu wa 2013 umegharamiwa na Benki ya
Maendeleo ya Kiislamu { Badea } kwa kushirikiana na SMZ kwa kiasi cha
Shilingi za Kitanzania Bilioni 14,834,615,889.06/-.
Akitoa
maelezo Mshauri muelekezi wa Mradi huo kutoka kampuni ya Newtech Consulting
Group ya Nchini Sudan El-Tayeb Rabah Mohammed alisema kuwa mradi huo umepangwa
kuchukuwa takriban miezi 17 hadi kukamilika kwake mwezi Mei mwaka ujao.
El –
Tayeb alimuhakikishia Makamau wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwamba
ana matumaini makubwa ya kupatikana kwa kiwango kizuri cha ujenzi
kitakachokidhi mahitaji yaliyokusidiwa kwa pande zote mbili.
Alieleza
kuwa Wataalamu hao wa ujenzi wameshasafisha eneo la wastani wa Kilo mita 10 na
kufanya kazi za kutengeneza Tabaka la Chini kwa wastani wa Kilo mita mbili kwa
Bara bara ya Cheju –Jendele – Kaebona.
Wizara
ya Miundo Mbinu na Mawasiliano Zanzibar ilitilianasaini Mkataba na Kampuni ya
DP Shapriya + Co Ltd ya Dar es salaam kwa kazi za utekelezaji wa ujenzi wa Bara
bara tatu za Vijijini Unguja mnamo tarehe 11 Septemba mwaka 2012.
Kukamilika
kwa bara bara hizo na hasa ile ya Cheju-Jendele- Kaebona kwa kiasi
kikubwa itawaondoshea usumbufu wakulima wa zao la mpunga ambao walikuwa
wakipata usumbufu kwa miaka kadhaa sasa
Na
Othman
Khamis Ame,
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar
*ASANTE KWA KUTEMBELEA BLOG YETU*
*ASANTE KWA KUTEMBELEA BLOG YETU*
0 comments:
Post a Comment