Breaking News

Tuesday

UJIO WA JAJI MUTUNGI BAADA YA JOHN TENDWA..


Ban Ki Moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alipata kusema; “Tatizo kubwa kwa nchi za Afrika si nakisi kwenye bajeti zao, bali, nakisi ya IMANI”.
Na Profesa Gaudence Mpangala naye amepata kusema; “ Msingi wa matatizo yetu mengi ni uwepo wa mfumo wa Chama Dola.”Na kwangu mimi, changamoto kubwa kwa Katiba yetu ijayo ni kuona kama itatoa nafuu ya hayo mawili hapo juu.
Maana, haiyumkini tukafanikiwa kujenga taifa la kisasa kamatutakosa ujasiri wa kuzipa  mgongo  kanuni na taratibu za kijima kwa maana ya taratibu  za kizamani.

Jakaya Kikwete ameonyesha kuwa mfano wa kiongozi mwenye ujasiri wa kuzipa mgongo kanuni na taratibu za kijima. Swali, ni wangapi wengine kwenye mfumo anaoutumikia wenye mitazamo kama ya kwake? Maana, maamuzi mengine ya kimageuzi anayoyafanya Kikwete yasingeweza kufikiriwa miaka kumi iliyopita.
Jana Jakaya Kikwete amefanya uteuzi wa Jaji  Francis Mutungi  kushika nafasi ya John Tendwa kama Msajili wa Vyama. Ukweli unabaki, kuwa kwenye utendaji wake, Tendwa kama mlezi hakuaminika na baadhi ya aliowalea. 
Hilo ni pungufu kubwa na linakwaza juhudi za kukuza demokrasia ya nchi. Msajili wa vyama vya siasa anapaswa aonekane kuwa ni  mlezi wa vyama vya siasa na wala si mwonezi wa vyama vya siasa. Na kazi ya ulezi inatakiwa ionekane.

Miaka 20 iliyopita nilipata bahati ya kukutana  na Msajili wa kwanza wa Vyama Vya Siasa. Ni Bw. George Liundi. Ni mwaka 1993, ilikuwa ni katika mwaka wake wa kwanza kama Msajili. Nakumbuka vema, nikiwa kijana mdogo tu, George Liundi alinipokea kwenye ofisi zake pale Mtaa wa Shaaban Robert. Tulikunywa chai na kuongea kwa kirefu.
Sijui George Liundi yuko wapi siku hizi, hakika ningependa nikutane nae nimkumbushe juu ya mazungumzo yetu yale. Maana, baadhi ya changamoto za mfumo wa vyama vingi tulizoziongea na Bw. Liundi miaka 20 iliyopita ndio  zinazoonekana sasa.
Nakumbuka Liundi alikuwa mtu muwazi sana. Alionyesha  hata wakati huo, wasiwasi wake  juu ya vyama kufichaficha mambo yao ya ndani na kuwa vingine vilikuwa ni kama NGO ya mtu au kikundi cha watu.  Kwamba kulikuwa na tatizo la uwepo wa demokrasia ya ndani ya vyama- Intra party democracy.
Hata wakati ule, niliona kupitia mazungumzo yangu  na Liundi, kuwa dhana ya kuwa Msajili wa Vyama ilionekana kwenye macho ya Chama Dola na jamii kwa ujumla kuwa ni kuwa mlezi wa vyama vinavyoanzishwa. Kwamba CCM ni chama kikongwe na hakikuhitaji ‘ kulelewa’ na Msajili.
Kwa wakati huo vyama vilivyosajiliwa havikuonekana kuwa na impact sana na hata kuwa tishio kwa CCM. Vingi vilikuwa kwenye ugomvi wa ndani kitu ambacho CCM kwa wakati huo haikuwa kabisa na tatizo hilo.
Nilichokipata kwenye mazungumzo yangu na Liundi miaka 20 iliyopita ni ukweli,  kuwa hakukufanyika review ya kina juu ya katiba za vyama kabla ya kusajiliwa. Ndio maana, masuala kama haya ya vyama kuwa na vikosi au vikundi vyake vya ulinzi yalipaswa kupigwa marufuku na Msajili tangu wakati huo bila kujali kama CCM wana Green Guards.

Na hii kwa kweli ndio moja ya changamoto ya Jaji  Francis Mutungi. Kuwa anakwenda pale Mtaa Shaaban Robert kushika ofisi yenye dhamana ya kuwa mlezi wa vyama vyote vya siasa nchini, ikiwamo CCM.
Na hatari hii ya vyama kuwa na vikosi au vikundi vya ulinzi bila shaka naye atakuwa ameshaiona, kuwa ni moja ya mambo yanayoweza kuchochea vurugu na kuvunja amani ya nchi. Kwamba vyama vifanye kazi ya siasa na kuendesha mafunzo ya siasa kwa vijana wake, na kamwe si mafunzo ya kijeshi.
Ikiwezekana Jaji Mutungi mwenyewe aandae muswada wa sheria ili ufikishwe bungeni. Sherkia ya kupiga marufuku ya vyama vya siasa kujihusisha na masuala ya kijeshi.  Na vyama vyenye kukiuka sheria hiyo vifutwe, kwa mujibu wa sheria.
Na hakika, miaka 20 baaada ya kuongea na Bw. George Liundi, nitapenda sana kukutana na kuongea na Jaji Mutungi kwenye mwaka wake wa kwanza wa utumishi wa umma kama mlezi wa vyama vya siasa. Kila la kher Jaji Francis Mutungi.
Na Maggid Mjengwa,
Share:

0 comments:

Post a Comment

Chapisho Lililoangaziwa

WEDDING PARTY PHILLIPO AND LUSIO

PHILLIPO & LUSIO WEDDING PARTY: STILL PICTURE, VIDEO SHOOTING MC & MUSIC BY MC SIMBA COMPANY 0715 501 059

Jumla ya Mara Iliyotazamwa

Powered by Blogger.

Pages